MWAUWASA kuendeleza ushirikiano na Jamii

Posted On: Apr 24, 2020


MWAUWASA KUENDELEZA USHIRIKIANO NA JAMII

USHIRIKIANO na Jamii ni nyenzo muhimu ambayo hutumiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) katika uendeshaji wa shughuli zake.

Kupitia ushirikiano huo na Jamii, MWAUWASA imefanikiwa kupunguza kero mbalimbali kwenye maeneo inayofikisha huduma kwani changamoto nyingi zinapata ufumbuzi kupitia ushirikiano huo wa pamoja.

“Tunafanya kazi kwa kushirikiana na Jamii, tunajadili kwa pamoja changamoto mbalimbali hususan ya upungufu wa maji kwenye maeneo ya pembezoni kwa lengo la kupata ufumbuzi wa pamoja,” anasema Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele.

Utaratibu huu wa ushirikiano na Jamii pia unaratibiwa kupitia program ya ‘Zungumza na MWAUWASA’ ambayo ilianzishwa kwa ajili ya kujadiliana na wananchi juu ya kero walizonazo kwenye suala zima la huduma ya maji.

Programu hii ni endelevu na inaendeshwa kwa mpango wa mikutano ambayo huitishwa na Wenyeviti wa Mitaa kwa kushirikiana na MWAUWASA.

Faida ya Programu hii ni pamoja na Mwananchi kupata fursa ya kueleza kero kuhusiana na suala zima la huduma ya maji; Kupata utatuzi/ufumbuzi wa pamoja wa kero; Mwananchi kupata elimu ya masuala mbalimbali yanayohusu maji na Mwananchi kupata fursa ya kuelewa shughuli zinazofanywa na MWAUWASA