News

Posted On: May, 14 2020

MWAUWASA yatunukiwa cheti cha ushindi kwa huduma nzuri

News Images

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) imetunukiwa cheti cha ushindi wa tatu katika utoaji wa huduma nzuri za majisafi na usafi wa mazingira kwa Mwaka 2018/19 katika kundi la Mamlaka za Maji za Mikoa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ewura ya Mwaka 2018/19, Mamlaka za Maji za Mikoa zilizoibuka kinara katika utoaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira ni Mamlaka ya Maji Moshi ambayo imeshika nafasi ya kwanza, Mamlaka ya Maji Iringa ambayo imeshika nafasi ya pili na Mamlaka ya Maji Mwanza ambayo imeshika nafasi ya tatu.

Akizungumza Ofisini kwake Jijini Mwanza Mei 13, 2020 wakati wa hafla ya utoaji wa cheti kwa MWAUWASA, Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Ziwa, George Mhina alisema uzinduzi wa taarifa za Mamlaka za Wilaya na Miji na ile ya Mamlaka za Mikoa na Miradi ya Kitaifa ulikuwa ufanyike Dar es Salaam hata hivyo alisema haukuweza kufanyika kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Corona (COVID 19).

“Katika kuchukua tahadhari dhidi ya COVID-19 na ili kuepuka mikusanyiko ya watu wengi; iliamuliwa Mamlaka zilizofanya vizuri zipokee tuzo na vyeti kupitia ofisi za kanda za EWURA nchini kote tofauti na ilivyokuwa inafanyika katika miaka iliyopita kwa viongozi wa Mamlaka za Maji zote kukutana kwenye mkutano wa pamoja wa mwaka,” alifafanua Mhina.

Mhina alivitaja vigezo vilivyotumika kushindanisha Mamlaka za Maji kuwa ni kiwango cha maji yanayozalishwa, idadi ya wananchi wanaopata huduma, ubora wa maji, idadi ya wateja wa huduma ya majisafi na mtandao wa uondoshaji majitaka, uwiano wa watumishi na idadi ya wateja sambamba na ufanisi wa ukusanyaji wa maduhuli.

Aidha, Mhina aliipongeza MWAUWASA kwa kushika nafasi hiyo ya tatu kati ya Mamlaka 26 zinazotoa huduma kwenye Makao Makuu ya Miji Mikuu ya Mikoa.

Akielezea taarifa ya Ewura 2018/19 Mhina alisema inadhihirisha Mamlaka za Maji zinaendelea kufanya vizuri ikilinganishwa na taarifa za kipindi cha nyuma huku akitolea mfano maeneo ambayo Mamlaka zimeongeza ufanisi ikiwemo kuongezeka kwa kiwango cha maji yanayozalishwa, kuongezeka kwa idadi ya wateja na kuimarika kwa ubora wa maji.

Mhina alisisitiza kuwa licha ya kuwepo kwa mafanikio yaliyoonyeshwa na Mamlaka nyingi za maji zipo changamoto zinazohitaji ufuatiliajia wa karibu zaidi ambazo ni pamoja na upotevu mkubwa wa maji, kukosekana kwa mifumo ya majitaka kwenye baadhi ya mamlaka na changamoto ya weledi miongoni mwa baadhi ya wataalam kwenye baadhi ya Mamlaka.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele wakati akipokea cheti aliishukuru EWURA kwa mwongozo juu ya namna ya kuboresha upatikanaji wa huduma na aliahidi kufanya vizuri zaidi.

“Tunashukuru kwa kupata ushindi huu lakini tunaahidi kuongeza jitihada kwenye utendaji wetu wa kila siku ili kuimarisha upatikanaji wa huduma kwenye maeneo tunayoyasimamia,” alisema Mhandisi Msenyele.