News

Posted On: Jun, 12 2020

​Taasisi za kijamii kupelekewa huduma ya maji – Prof. Mkumbo

News Images

Taasisi za kijamii kupelekewa huduma ya maji – Prof. Mkumbo

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo amesema Serikali imedhamiria kupelekea huduma ya maji kwenye taasisi zote muhimu za kijamii kote nchini.

Amesema hayo Juni 10, 2020 wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa Wilayani Chato Mkoani Geita akiwa ameambatana na Naibu wake, Mhandisi Anthony Sanga.

Profesa Mkumbo amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais. Dkt. John Pombe Magufuli ni kuhakikisha taasisi mbalimbali muhimu ikiwemo vituo vya afya, zahanati na shule zinapata maji ili kurahisisha na kuboresha utoaji wa huduma zinazotolewa na taasisi hizo ikiwa ni pamoja na kuondokana na kutembea umbali mrefu kwa wanufaika wake.

“Mwaka huu kwenye bajeti yetu, Serikali imedhamiria kuondokana na kero ya maji kwenye taasisi muhimu za kijamii zikiwemo taasisi za afya na elimu na kwa kutambua hili tumetenga fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maji kwenye taasisi hizi kote nchini,” alifafanua Profesa Mkumbo.

Akielezea utekelezaji wa miradi ya maji wilayani humo, Profesa Mkumbo anasema kuna miradi mitatu inatekelezwa ambayo kati yao mmoja umeanza kutoa huduma, mwingine umeanza kutekelezwa Juni 9, 2020 na huku mwingine mkubwa na ambao anasema ni mwarobaini kwa kero ya maji wilayani humo utekelezwaji wake utaanza hivi karibuni kwani ulisimama kutokana na janga la corona.

Aliitaja miradi hiyo kuwa ni mradi wa maji wa Imalabupina Ichwankima ambao umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 8.2 ambao anasema umekamilika na tayari vijiji 3 vinapata huduma ya maji, mradi mwingine ni wa uboreshi huduma ya maji kwenye mji wa Chato ambao pia utapelekeka huduma kwenye uwanja wa ndege wa Chato mbao umeanza kutekelezwa Juni 9, 2020 na unatekelezwa na wataalam wa ndani kwa gharama ya shilingi bilioni 4.

Anafafanua kwamba mradi huo wa uboreshaji huduma kwenye mji wa Chato unahusisha uboreshaji wa chanzo cha maji, ulazaji wa bomba kutoka kwenye chanzo cha maji hadi kwenye matenki, ujenzi wa matenki mawili ya lita 225,000 na lita 90,000.

Profesa Mkumbo anaongeza kuwa program nyingine ya maji ambayo inatekelezwa pia kwenye maeneo mengine kote nchini ni kupelekea huduma kwenye taasisi za kijamii ambayo nayo inatekelezwa na wataalam wa ndani na anabainisha kwamba kwa wilayani humo kwa mwaka huu wa fedha inahusisha uchimbaji wa visima kwa ajili ya shule 19 na tayari imeanza kutekelezwa na shule zipatazo 5 zimechimbiwa visima na kwa sasa kisima kinachimbwa kwenye shule ya Sekondari ya Ilemela wilayani humo.

Akizungumzia mradi mkubwa wa maji wa Shilingi Bilioni 500 ambazo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India, Profesa Mkumbo anasema utanufaisha miji mbalimbali ikiwemo Geita, Chato na Kayanga Mkoani Kagera ambao hata hivyo anabainisha kwamba umechelewa kuanza kutekelezwa kutokana na janga la corona lililoikumba dunia.

Hata hivyo anabainisha kwamba mradi huo mkubwa utekelezwaji wake utaanza hivi karibuni baada ya makali ya janga hilo kupungua na kwamba tayari Wakandarasi wengi wameonesha nia na wameanza kutuma maombi ya kutekeleza miradi hiyo ambayo anasema kwa Mji wa Chato mradi utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 45.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akizungumzia utekelezwaji wa miradi wilayani humo anasema unazingatia kasi ya ukuaji wa mji wa Chato na kwamba lengo ni kuwa na huduma ya ziada ya maji itakayokwenda sambamba na ukuaji wa mji huo.

Mhandisi Sanga anasema miradi ambayo imeanza na inaendelea kutekelezwa wilayani humo ni ya muda mfupi na kwamba mradi huo wa bilioni 45 ambazo ni fedha kutoka India ndio pekee utakaomaliza tatizo la maji mahala hapo kwani utawezesha kujengwa mradi mkubwa zaidi kuliko yote inayojengwa hivi sasa hapo Chato.

Anasema miradi iliyopo hivi sasa inao uwezo wa kuzalisha kiasi cha lita 1,350,000 ambayo ni sawa na asilimia 23 pekee kwa siku na kwamba maboresho yanayofanyika sasa kama ilivyobainishwa hapo awali na Profesa Mkumbo yataongeza kiasi cha lita 3,200 kwa siku na hivyo kufikisha asilimia 56.5 tu ya upatikanaji wa huduma kwa siku.

Mhandisi Sanga anabainisha kwamba lengo ni kufikia asilimia 100 na kwamba ili kuifikia ni kupitia mradi huo mkubwa utakaotekelezwa kwa kutumia fedha za India ambao anasema utamaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa Mji wa Chato.

“Huu mradi wa bilioni 45 ni mradi mkubwa na ni kama miradi mingine tuliyotekeleza Sengerema, Magu, Nansio na Lamadi na huu mradi ndio hasa mwarobaini wa kero ya maji kwa Mji huu wa Chato,” anafafanua Mhandisi Sanga.

Mhandisi Sanga aliwasisitiza wataalam wanaotekeleza mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji kwenye Mji wa Chato kuhakikisha wanaongeza nguvu kazi ili kukamilisha mradi kwa wakati hasa ikizingatiwa kwamba tayari fedha ya utekelezaji imetengwa na nyingine imekwishatolewa.

"Hakuna sababu ya kuchelewesha mradi, fedha ipo, vifaa vipo, ongezeni nguvu kazi ya wachimba mtaro na tena mtoe kipaumbele kwa wenyeji wa maeneo haya ili mradi ukamilike mapema iwezekanavyo," alielekeza Mhandisi Sanga.

Aidha, kupitia ziara hiyo, ya siku moja, Katibu Mkuu na Naibu wake walipata fursa ya kuhudhuria Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Chato ambapo walielezea juu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kwa Mwaka 2015-2020 katika Sekta ya Maji kwenye Halmashauri hiyo.

Wajumbe wa Baraza hilo akiwemo Mbunge wa Jimbo la Chato ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani waliipongeza Wizara ya Maji kwa jitihada inazoendelea nazo za kuhakikisha kero ya maji kwenye Halmashauri hiyo inakuwa historia

Hata hivyo walisisitizwa kuhakikisha wanaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo inayoendelea kutekelezwa ili kwenda sambamba na kasi ya ukuaji wa Halmashauri hiyo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo akishiriki kwenye uchimbaji wa mtaro wa kulaza bomba la maji kutoka kwenye chanzo hadi uwanja wa ndege wa Chato.

Uchimbaji wa kisima kwenye shule ya Sekondari ya Ilemela Wilayani Chato ukiwa katika hatua za mwisho kama ilivyoonekana wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo (kulia) alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji Wilayani Chato. Katikati ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Anthony Sanga na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo (katikati) alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi wa kupeleka maji kwenye uwanja wa ndege wa Chato. Wa pili kulia ni Naibu wake, Mhandisi Anthony Sanga