News

Posted On: Feb, 18 2020

Tenki la Nyegezi Majengo Mapya limekamilika

News Images

Imeelezwa kuwa ujenzi wa tenki la maji la Nyegezi Majengo Mapya umekamilika, wananchi watarajie kuanza kupata huduma kupitia tenki hilo mwishoni mwa mwezi huu.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele amebainisha hilo Februari 14, 2020 kwenye ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dkt. Phillis Nyimbi na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya iliyolenga kujionea hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa tenki hilo.

Mhandisi Msenyele alisema ujenzi wa Tenki la Nyegezi Majengo Mapya umekamilika na kinachofanyika hivi sasa ni kuondoa uchafu (flushing) na vimelea (disinfection) kwenye mfumo wa mabomba ili kuwawezesha wananchi kupata maji safi na salama.

"Hivi sasa tupo kwenye hatua za disinfection na flushing na zoezi hili litachukua Siku Saba na baada ya hapo tukijiridhisha usalama wa maji tutayaruhusu kufika kwa wananchi," alisema Mhandisi Msenyele.

Alisema tenki hilo lenye uwezo wa kuhifadhi lita 1,200,000 za maji litahudumia wananchi wa Nyegezi Majengo Mapya, Mkolani na Buhongwa huku taratibu za ujenzi wa mradi mwingine mkubwa wa chanzo kipya cha maji hapo Butimba zikiendelea.

Aliongeza kuwa chanzo hicho cha maji kinachotarajiwa kujengwa hapo Butimba kitaimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwenye maeneo yote yenye changamoto.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dkt. Phillis Nyimbi aliipongeza MWAUWASA kwa usimamizi wa mradi na alipongeza hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa tenki hilo.

Akielezea lengo la ziara yake kwenye tenki hilo, Dkt. Nyimbi alisema ni kufuatilia maelekezo ya Serikali kwenye ujenzi wa miradi inayotekelezwa kwa fedha za walipakodi.

"Tumekuja leo kwa ajili ya kufuatilia maelekezo ya Serikali yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso wakati wa ziara yake hapa kwenye tenki Januari 8, 2020 ambapo aliagiza Mkandarasi awe amekamilisha mradi huu ndani ya wiki mbili kuanzia tarehe hiyo ya ziara yake,"alisema.

Alipongeza hatua aliyoikuta na alimsisitiza Mkandarasi Kampuni ya JR International kuhakikisha anakamilisha kama ilivyoelekezwa.

"Ni jukumu letu sisi kama viongozi kuhakikisha miradi hii ambayo inajengwa kutokana na fedha za wananchi walipakodi inatekelezwa kama inavyotakiwa," alisema.

Tenki hilo la Nyegezi Majengo Mapya ni miongoni mwa matenki 6 ambayo yanatekelezwa chini ya Programu ya Uboreshaji wa Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Jiji la Mwanza, Miji ya Bukoba na Musoma, Miji Midogo ya Misungwi, Magu na Lamadi (LV WATSAN).

Matenki mengine yaliyotekelezwa chini ya programu hiyo ya LV WATSAN Jijini Mwanza chini ya usimamizi wa MWAUWASA ni matenki ya Kitangiri, Nyasaka, Mjimwema, Bugarika na Nyamhongolo.