News

Posted On: Apr, 14 2020

Watumishi MWAUWASA watakiwa kuboresha utendajikazi

News Images

KAIMU Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele amemtaka kila mtumishi wa Mamlaka hiyo kutambua wajibu wake wa kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mhandisi Msenyele ametoa maelekezo hayo hapo jana (Aprili 8, 2020) Wilayani Kwimba akiwa ameambatana na Menejimenti ya MWAUWASA kwenye kikao chake cha kwanza na watumishi wa Kanda ya Ngudu kilicholenga kujadili mwelekeo wa pamoja wa utoaji huduma kwa wananchi wa Mji wa Ngudu na viunga vyake.

Kanda ya Ngudu ni miongoni mwa Kanda mpya zilizo chini ya MWAUWASA kufuatia hatua yenye maelekezo ya Serikali kupitia Wizara ya Maji kuiongezea wigo wa eneo la usimamizi katika utoaji wa huduma za Majisafi na Usafi wa Mazingira hadi katika miji ya Ngudu, Magu, Nansio na Misungwi kama ilivyotangazwa rasmi kwenye Gazeti la Serikali GN Na. 670 la Septemba 6, 2019 na GN Na. 70 la Januari 31, 2020.

Maelekezo ya maboresho hayo yalilenga kuimarisha uendeshaji wa Sekta ya Usambazaji maji na usafi wa mazingira mijini ambapo hapo awali kabla ya mabadiliko hayo Kanda ya Ngudu ilikuwa ikitambulika kama Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Ngudu (NGUWASA).

Mhandisi Msenyele alisisitiza kuwa kila mtumishi anapaswa kutambua umuhimu wa Sekta ya Maji kwa jamii anayoihudumia hasa ikizingatiwa kwamba maji hayana mbadala na kwamba ni jukumu la kila mtumishi kuhakikisha anatekeleza wajibu wake ipasavyo.

“Mnapaswa kuelewa huduma ya maji inahitajika kwa kila mwananchi, hakuna maisha bila maji kwahivyo hampaswi kuzembea katika hili, nami siwezi kuvumilia kuona mtumishi anashindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu,” alisisitiza.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, watumishi wa Kanda hiyo ya Ngudu walieleza changamoto mbalimbali wanazopitia ikiwemo uchakavu wa miundombinu inayosababisha upotevu wa maji, madeni yanayoikabili kanda hiyo na huku baadhi ya taasisi zikishindwa kulipia huduma kwa wakati.



Akizungumzia changamoto hizo, Mhandisi Msenyele aliwahakikishia watumishi hao ushirikiano wa kutosha katika kuzipatia ufumbuzi wa kudumu huku akisisitiza maeneo nyeti wanayopaswa kufanyia kazi ili kuondokana na changamoto walizobainisha.

“Changamoto mlizotueleza inawezekana kabisa kuziondoa kama tutafanya kazi kwa ufanisi kama kusoma dira za maji kwa wakati na kwa kila mteja, kufuatilia madeni sambamba na kuhakikisha huduma inapatikana wakati wote. Tukiongeza ufanisi wa ufanyaji kazi tutaboresha huduma zetu na wakati huohuo tutapunguza changamoto zinazotukabili,” alibainisha.

Alisisitiza kuwa kila Kanda inapaswa kujiendesha kwa kutumia mauzo yake na kwamba suala hilo litafanikiwa endapo tu kila mtumishi atafanya kazi kwa bidii na ushirikiano, atakubali kukosolewa pale mambo yatakapokwenda tofauti na inavyopasa.

“Kaulimbiu yetu ni kumtua mama ndoo kichwani sasa ni vipi tutamtua ndio huko kuhakikisha huduma inaimarika, umuhimu wa kuhakikisha tunauza maji tunayozalisha na pia kuhakikisha tunachokiuza tunakikusanya. Nia tunayo uwezo tunao na sababu tunazo za kuhakikisha mauzo yanapanda," alisisitiza Mhandisi Msenyele.

Aidha, aliwatoa hofu watumishi hao kuhusiana na suala zima la ajira zao ambapo aliwahakikishia kuendelea na nafasi za ajira walizonazo na kwamba maboresho zaidi yatafanyika ili kuhakikisha kila mtumishi anamudu vyema majukumu yake.

“Pamoja na mabadiliko yaliyotokea niwatoe hofu hakuna atakayepoteza ajira yake na mtaona uzuri wa kufanya kazi chini ya MWAUWASA. Ninawahakikishia Serikali ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kupitia Wizara ya Maji imefanya haya kwa nia njema ya kuboresha huduma na si vinginevyo,” alifafanua Mhandisi Msenyele.

Kwa upande wake Meneja wa Utawala na Rasilimali Watu wa MWAUWASA, Deogratius Magayane alizungumzia muundo utakaotumika kwenye uendeshaji wa Kanda hiyo na alimtaka kila mtumishi kuhakikisha anauelewa vyema ili kuepuka mgongano wa kimajukumu.

Alisisitiza suala zima la nidhamu kwa kila mtumishi na aliwakumbusha kuepuka vitendo vya rushwa, kuepuka matumizi ya lugha na tabia zinazokiuka maadili ya utumishi wa umma. “Nidhamu muhimu ikazingatiwa, suala la rushwa tulipige vita ikumbukwe kuwa hakuna rushwa ndogo kwani rushwa ni rushwa tu, tudhibiti hasira zetu tunapokutana na wateja tuhakikishe tunatumia kauli zenye kujenga,” alisisitiza.

Naye Meneja Biashara wa MWAUWASA, Meck Manyama alisisitiza ushirikiano na aliwataka watumishi hao kuepuka kukaa maofisini badala yake wahakikishe wanawatembelea wateja wao ili kubaini hali ya huduma, kujadili changamoto zinazowakabili wateja na kuzipatia ufumbuzi wa haraka kwa lengo la kuongeza mauzo na makusanyo.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Meneja wa Fedha MWAUWASA, Nyanjige Petro na Mtaalamu wa masuala ya Tehama, Maleva Kaduma kwa lengo la kutoa ufafanuzi wa masuala ya kifedha na Tehama katika kuboresha huduma.

Katika kikao hicho, Mhandisi Msenyele alimteua Juma Saidi (Afisa Usambazaji Maji MWAUWASA) kuwa Mkuu wa Kanda ya Ngudu baada ya aliyekuwa Mkuu wa kanda hiyo, Mhandisi Mapengu Gendai kuhamishiwa Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).