News

Posted On: Apr, 18 2024

KAMATI YA SIASA NYAMAGANA YAIPONGEZA MWAUWASA

News Images

KAMATI YA SIASA NYAMAGANA YAIPONGEZA MWAUWASA

Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Nyamagana imeipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kwa utekelezaji mahiri wa miradi inayolenga kuimarisha upatikanaji wa huduma ya Majisafi na uimarishaji wa Usafi wa Mazingira kwa wananchi.

Pongezi hizo zimetolewa wakati wa ziara ya Kamati hiyo ilipotembelea na kujionea utekelezaji wa mradi wa kuboresha huduma ya maji maarufu kama mradi wa matokeo ya haraka (quick win) Aprili 18, 2024 katika Kata ya Luchelele pamoja na Mtambo wa uchakataji Majitaka (DEWATS) katika Gereza la Butimba.

Kamati hiyo iliambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi imesema MWAUWASA imefanya kazi nzuri na inayoridhisha katika utekelezaji wa miradi hiyo inayoenda kuleta manufaa kwa wakazi wa maeneo husika.

"Kwanza tumpongeze Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA, kwakweli tangu amefika tunaona jitihada za kila siku za kuhakikisha huduma inaimarika, mara kadhaa mimi mwenyewe tumekua tukiwasiliana na umekua ukiwafikia wananchi na kupokea changamoto kwaajili ya kuzipatia ufumbuzi, tunakupongeza kwa hili," amesema Mhe. Peter Begga Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Nyamagana

Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe Amina Makilagi amesema pamoja na pongezi hizo Serikali kupitia Watumishi wake itaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

"Kwa niaba ya Serikali tunapokea pongezi hizi za Chama, nami niseme tu Watumishi wa Serikali ikiwemo taasisi hii ya MWAUWASA tutaendelea kuchapa kazi kwa pamoja ili kutimiza azma ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani," amesema Mhe. Makilagi

Aidha, akizungumza mbele ya Kamati hiyo Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA Ndg. Neli Msuya amesema MWAUWASA inaendelea na jitihada za kuhakikisha huduma inafika katika maeneo yote ambayo yalikua hayajafikiwa kikamilifu.