News
UBORESHAJI HUDUMA YA MAJI BUHONGWA, MABOMBA YAANZA KUPOKELEWA
Katika kuendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji jijini Mwanza, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) imeanza kupokea mabomba kwaajili ya utekelezaji wa mradi mpya utakaoleta matokeo ya haraka unaokusudia kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa kata ya Buhongwa Wilayani Nyamagana.
Shehena hiyo ya bomba iliyopokelewa Julai 25, 2024 inaashiria kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo utakaohusisha ulazaji wa bomba litakalotoa maji tenki la Sahwa ili kuongeza wingi wa Maji yanayowafikia wakazi wa kata ya Buhongwa kwa zaidi ya lita Milioni nane (08) kwa siku.
Aidha, mbali na mradi huo wa dharura MWAUWASA ina mpango wa utekelezaji wa mradi wa uboreshaji mtandao wa maji kwa kata za Buhongwa, Mkolani na Luchelele Kwa gharama ya TZS Billion 1.88 ambao utanufaisha wakazi wa maeneo ya Buhongwa, Bulale - Kigoto, Msufini, Shibai, Sahwa ya chini, Mkolani, Nyahingi, Buguku na Luchelele. Mradi huu utagharamiwa na Serikali kupitia Wizara ya Maji.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA Neli Msuya ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji chini ya Waziri Mhe. Jumaa Aweso (Mb) kwa kuiwezesha Mamlaka kuendelea na jitihada zinazofanyika kuimarisha huduma ya maji kwa wakazi wa Mwanza kama ilivyo dhamira ya Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani.
'Tayari pampu ipo na tumeanza kupokea mabomba. Kazi ya ulazaji mabomba kwa kilometa 4.5 tutaifanya haraka ili kuhakikisha tunaleta ahueni haraka katika eneo la Buhongwa,"
Akizungumza na Naibu Waziri wa Maji Mhe. Kundo Mathew ambaye yupo ziarani Mkoani Mwanza alisema Mamlaka sasa imeelekeza jitihada zake katika uimarishaji wa miundombinu ya usambazaji maji ili maji yanayozalishwa yaweze kuwafikia wananchi kikamilifu.
#Tumejipanga_tupo_tayari_kuwahudumia💦