News

Posted On: Jun, 30 2020

​RC Mongella aimwagia sifa MWAUWASA

News Images

RC MONGELLA AIPONGEZA MWAUWASA

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella ameipongeza MWAUWASA kwa utekelezaji wake wa miradi ya maji ikiwemo mradi wa ujenzi wa tenki la Majisafi kwenye Mji wa Ngudu, Wilayani Kwimba.

Ametoa pongezi hizo Juni 27, 2020 wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Hospitali na Chuo cha VETA Wilayani Kwimba.

Mongella alimpongeza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele kwa jitihada zake za kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

“Hongera sana Kaimu Mkurugenzi, Mhandisi Msenyele; mnafanya kazi nzuri kwa manufaa ya wananchi, hii inatia moyo na kupitia mradi huu ni Imani yangu kwamba wananchi watanufaika kwa kuondokana na kero ya upatikanaji wa maji waliyokuwa nayo,” alisema Mongella.

Akielezea utekelezaji wa mradi, Mhandisi Chacha Mwita alisema mradi unatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 490 (490,845,470.84) ambazo zinatolewa na Serikali kupitia Wizara ya Maji na kwamba unatarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu.

“Hili tenki uwezo wake ni kuhifadhi kiasi cha lita milioni mbili na linapata maji kutoka KASHWASA kwa ajili ya kuhudumia wananchi wa Ngudu wapatao 37,000,” alisema Mhandisi Mwita.

Mhandisi Mwita alibainisha kwamba ujenzi wa tenki hilo umefikia silimia 80 na kwamba utekelezaji wake unakwenda kwa kasi ili kuhakikisha wananchi wanaanza kunufaika.

Ziara ya Mkuu wa Mkoa Mongella Wilayani Kwimba ni muendelezo wa ziara anazofanya za ukaguzi wa utekelezaji wa miradi mbalimbali kote Mkoani Mwanza kwa utaratibu aliyojiwekea wa ukaguzi wa miradi.Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella akizungumza wakati wa ziara yake kwenye mradi wa ujenzi wa tenki la maji katika Mji wa Ngudu, Wilayani Kwimba. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele

Ujenzi wa tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni mbili za maji Wilayani Kwimba ukiendelea kama inavyoonekana wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella (hayupo pichani)